Korea Kaskazini yashutumu mpango wa utaratibu mpya wa kufuatilia vikwazo

Korea Kaskazini imezishutumu Marekani, Japani na nchi zingine kwa kutoa ahadi ya pamoja ya kuunda utaratibu mpya wa kufuatilia vikwazo vya nchi hiyo.

Balozi wa Korea Kaskazini katika Umoja wa Mataifa Kim Song amekosoa hilo jana Jumapili kupitia Shirika la Habari la Serikali ya Korea Kaskazini la Korean Central.

Jopo la wataalam la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefuatilia utekelezaji wa vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini kwa miaka 15.

Lakini mamlaka yake yamemalizika Aprili 30 baada ya Urusi kupiga kura ya turufu kupinga azimio la kuendelea kwake.

Hali hiyo imesababisha Umoja wa Ulaya na nchi 49 kutoa taarifa ya pamoja siku iliyofuata iliyotoa wito wa utaratibu mpya wa kuchukua nafasi ya jopo hilo la Umoja wa Mataifa.

Vyanzo vya habari vyenye taarifa juu ya Korea Kaskazini vimeiambia NHK kuwa kumalizika kwa shughuli za jopo hilo la Umoja wa Mataifa kutarahisisha biashara ya Korea Kaskazini na kuiwezesha nchi hiyo kusafirisha bidhaa zaidi, zikiwemo rasilimali za ardhini.

Wataalam wana mashaka kwamba Korea Kaskazini itazidisha ukiukaji wake wa vikwazo.