Kishida agusia mafanikio katika ziara ya Ufaransa, Amerika Kusini

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio anakaribia kuhitimisha ziara yake ya siku sita nchini Ufaransa, Brazil na Paraguay. Na amegusia kile alichokifanikisha katika ziara yake.

Waziri Mkuu Kishida alifanya mkutano na wanahabari jijini Sao Paulo.

Kishida alisema: “Ni muhimu kuonesha kwa dhati dhamira zetu katika kuendeleza utaratibu huru na wazi wa kimataifa kulingana na utawala wa sheria, na kupanua wigo wa ushirikiano. Nilizingatia masuala na mazingira yanayokabiliwa na kila taifa, na kuchukua hatua za kina ambazo ni za kipekee kwa Japani, na kuzingatia mambo haya wakati wa ziara hii.”

Waziri mkuu huyo wa Japani alizungumza kwanza kuhusiana na ziara yake jijini Paris. Huko alihutubia Baraza la Mawaziri la Taasisi ya Ushirikiano na Maendeleo ya Kiuchumi.

Pia walikubaliana kwenye taarifa inayounga mkono kanuni na mapendekezo ya matumizi ya teknolojia ya akili bandia.

Kishida pia alikutana na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.

Katika uhusiano wa mataifa mawili na Ufaransa, Kishida alisema kwamba yeye na Macron waliweza kuweka msingi wa kuimarisha uhusiano wa kiusalama kati ya mataifa hayo mawili.

Kishida alisema: “Katika mkutano na Rais Macron, tulikuwa na mazungumzo ya kina juu ya hali ya sasa nchini Ukraine, Mashariki ya Kati na Asia Mashariki katika mahusiano ya mataifa mawili. Na tuliweza kutoa matokeo madhubuti kwa kukubaliana juu ya kuanza kwa majadiliano kuhusu Makubaliano ya Ubadilishanaji kati ya Japani na Ufaransa.”

Kisha Kishida alizungumza kuhusiana na ziara yake ya kwanza katika bara la Amerika Kusini kama waziri mkuu ili kuimarisha uhusiano kati ya Japani na nchi za “Global South.” Katika mkutano na Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva, viongozi hao walikubaliana juu ya Mpango wa Green Partership wa kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabia nchi.

Nchini Paraguay, alikutana na Rais Santiago Pena. Viongozi hao wawili walikubaliana kuongeza zaidi wigo wa ushirikiano na mabadilishano kati ya mataifa hayo mawili.

Waziri Mkuu Kishida aliahidi kuimarisha uhusiano na eneo lote la Amerika ya Kati na Kusini katika jamii anuai ya kimataifa.

Kishida alisisitiza kuwa aliweza kuwafikia viongozi wa dunia juu ya umuhimu wa kudumisha utaratibu huru na wazi wa kimataifa kwa kuzingatia utawala wa sheria.

Alisema: “Tutafanikisha dunia ambayo inalinda utu wa mwanadamu. Kuelekea hili lengo muhimu la pamoja, Japani itatoa ushirikiano wa kutosha ambao unawakilisha Japani, wenye utofauti na jumuishi kwa mataifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na yale ya Amerika Kusini na ya Kati.”

Kishida atarejea nchini Japani kesho Jumatatu.