Mazungumzo ya Gaza yaendelea lakini bado hakuna dalili dhahiri za makubaliano

Mazungumzo yameripotiwa kuendela katika mji mkuu wa Misri, Cairo kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka. Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kwamba Israel haitapeleka wajumbe huko Cairo hadi pale Hamas itakapokubali pendekezo la hivi karibuni.

Vyombo hivyo vya habari vimeripoti kwamba jana Jumamosi ujumbe wa Hamas na Mkurugenzi Mkuu wa CIA ya Marekani William Burns waliwasili nchini Misri. Misri inaratibu mazungumzo hayo.

Hamas ilisema itaingia katika meza ya majadiliano na mtazamo chanya ili kuweza kufikia makubaliano.

Vyombo vya habari vya Misri vilivinukuu vyanzo vya habari vya nchi hiyo vikisema masuala kadhaa yamefikiwa muafaka hadi sasa.

Pendekezo la hivi karibuni linajumuisha kusitisha mapigano kwa siku 40 ili kurejesha mateka kwa awamu na baadaye kuingia katika awamu inayofuata.

Bado haijawa bayana iwapo Hamas, inayodai usitishwaji mapigano kwa ukamilifu, na Israel ambayo inalenga katika kuiharibu Hamas, zitaweza kufikia maafikiano.

Wakati huo huo, Israel imeendelea kuishambulia Gaza licha ya majadiliano kuendelea.

Jana Jumamosi, vyombo vya habari vya eneo hilo viliripoti kwamba watu watatu wakiwemo watoto wawili waliuawa pale nyumba yao iliposhambuliwa kwa bomu mjini Rafah. Karibu Wapalestina milioni 1.2 wakiwemo wengi ambao walikuwa wamejihifadhi dhidi ya mashambulizi ya mabomu ya Israel kwenye maeneo mengine ya Gaza wapo mjini Rafah.

Mamlaka za afya za eneo hilo zinasema watu 34,654 wameuawa kwenye mgogoro huo wa sasa.