Wafanyakazi wa kujitolea watumia mapumziko ya msimu wa chipukizi kusaidia maeneo ya Japani yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi

Mkoa wa katikati mwa Japani wa Ishikawa unaendelea na ujenzi mpya kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililotokea Siku ya Mwaka Mpya lililoikumba Rasi ya Noto.

Jana Jumamosi, wanafunzi takribani 100 wa vyuo vikuu kutoka kote nchini Japani walijiunga na wakazi katika jitihada za kufanya usafi kwenye Mji wa Suzu ambapo tsunami ilisababisha uharibifu mkubwa.

Wakazi walielezea shukrani zao kwa msaada huo, wakisema “Hakuna lisilowezekana kama wote tukiungana.”

Kwenye mji ulioathirika vibaya wa Nanao, wakazi wa eneo hilo walivuna stroberi za Sakiyama, zinazolimwa katika eneo hilo.

Wakazi walilazimika kutegemea maji ya kisima yanayosafirishwa na lori kupanda mimea hiyo tangu pale usambazaji wa maji ya eneo hilo ulipositishwa takribani miezi mitatu iliyopita.

Mwanachama wa kundi la jumuiya ya Sakiyama, Kosaki Hirotoshi alisema alifurahia uvunaji. Aligusia kwamba licha ya kwamba stroberi ni ndogo kulinganisha na ukubwa wake wa kawaida, ni tamu zaidi.

Uharibifu uliosababishwa na tetemeko hilo uliwalazimisha wakazi kupunguza matukio ya kitamaduni kama vile tamasha la Seihakusai la eneo hilo ambalo kwa kawaida hufanyika katika kipindi hiki cha mwaka.

Gwaride la jukwaa kubwa lenye magurudumu linaloitwa Dekayama limetengwa na UNESCO kama Urithi wa Kitamaduni Usiogusika.

Lakini mwaka huu, gwaride hilo lilisitishwa kwa kuwa barabara zilizoharibika bado zinajengwa upya, wakati huu kukiwepo na wasiwasi wa usalama.

Mkuu wa chama cha hifadhi ya tamasha anasema wanalenga kufanya tamasha kamili msimu ujao wa chipukizi.