Benki ya Maendeleo Asia yaanza mkutano wa mwaka nchini Georgia

Mkutano wa mwaka wa Benki ya Maendeleo Asia ulianza rasmi jana Jumamosi katika mji mkuu wa Georgia Tbilisi.

ADB inajitolea kusaidia nchi za bara la Asia na Pasifiki kwa kutoa mikopo, ruzuku na msaada wa kiufundi kwa ajili ya miundombinu na miradi mingine.

Wakati wa hafla ya ufunguzi, Rais wa ADB Asakawa Masatsugu aligusia kuwa nchi masikini zaidi duniani na zenye watu wengi waliopo hatarini, ikiwa ni pamoja na watu wa mataifa ambayo ni visiwa, wanataabika kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, changamoto za kiuchumi na vita.

Alisisitiza kuwa hakuna mtu anapaswa kunyimwa matunda ya maendeleo. Asakawa alisema benki hiyo ipo tayari kuongeza kiwango cha msaada kinachotoa kwa nchi ambazo ni visiwa na mataifa mengine.

Waziri wa Fedha wa Japani Suzuki Shunichi leo Jumapili amepanga kutoa hotuba.

Suzuki anatarajiwa kutangaza kuwa Japani itatoa mchango kwa ADB, kwa kuwa benki hiyo inapanga kutoa fedha zaidi kwa mataifa yenye kipato kidogo.

Pia anatarajiwa kugusia kuwa Japani inadhamiria kuchangia katika juhudi zinazolenga kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na ujenzi wa miundombinu.