Rais Xi wa China apanga kuzuru katika mataifa matatu ya Ulaya

Rais Xi Jinping wa China atafanya majadiliano na viongozi wa Ulaya katika nchi tatu wakati wa ziara yake ya siku sita itakayoanza leo Jumapili.

Xi atasafiri kwenda Ufaransa, Serbia na Hungary. Itakuwa ni ziara ya kwanza ya kiongozi huyo wa China barani Ulaya katika kipindi cha miaka mitano.

Nchini Ufaransa, Xi amepangiwa kukutana na mwenzake wa nchi hiyo Emmanuel Macron. Watajadili uhusiano wa pande mbili na hali nchini Ukraine na Mashariki ya Kati.

Ziara hyo itaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Ufaransa.

Xi pia anatarajiwa kufanya majadiliano ya pande tatu nchini Ufaransa na Macron na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen. Watatu hao watajadili kuhusu mahusiano baina ya China na Umoja wa Ulaya.

Rais huyo wa China anatarajiwa kukutana na Rais Aleksandar Vucic huko Serbia. Pia atakutana na Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban nchini Hungary. Viongozi hao watajadili kile kilichofanikiwa kupitia Mpango wa Ukanda Mmoja na Njia Moja ya China.

Wizara ya Mambo ya Nje ya China inaamini kuwa ziara hiyo ya Xi itakuwa muhimu kwa uhusiano kati ya China na Ulaya. Pia inaamini kwamba ziara hiyo itachangia katika amani na maendeleo ya dunia.

Katika siku za hivi karibuni Xi alikutana na Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte nchini China.

China inaonekana kujaribu kuimarisha uhusiano wake na mataifa ya Ulaya kama njia ya kuifuatilia Marekani.

Nchi hizo mbili zipo katika mvutano juu ya usalama na teknolojia ya hali ya juu.