Israel yaendelea na mashambulizi huku makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza yakikwama

Ripoti ya vyombo vya habari inasema Israel imelipa kundi la Hamas wiki moja kukubaliana na mpango uliofanyiwa marekebisho wa kusitisha mapigano, vinginevyo itaanza operesheni ya kijeshi katika mji wa Rafah uliopo kusini mwa Gaza. Jarida la Wall Street lilinukuu maafisa wa Misri jana Ijumaa.

Misri imefanya kazi na Israel katika pendekezo lililowasilishwa kwa Hamas wikiendi iliyopita. Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh alisema wanalizingatia kwa "moyo chanya," lakini watatuma ujumbe nchini Misri hivi karibuni kwa majadiliano zaidi.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema yuko tayari kuendelea na mashambulizi ya ardhini huko Rafah "kukiwa au pasipo" na makubaliano. Mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa tayari yanajiandaa kwa uwezekano wa uvamizi.

Maafisa wanasema wanaanzisha vituo vya matibabu na vifaa katika mji wa Khan Younis na maeneo mengine ya Ukanda wa Gaza.

Bado, wanaonya mipango yao ya dharura ni "msaada wa muda" tu.

Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa UN, ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ONOCHA Jens Laerke, alisema mashambulizi yataweka mamia kwa maelfu ya watu katika "hatari ya karibu ya kifo." Ameongeza kuwa operesheni hiyo sio tu itakuwa "mauaji ya raia" bali pia "pigo kubwa sana" kwa operesheni za kibinadamu katika Ukanda wote wa Gaza.

Vyombo vya habari vya eneo hilo vinasema kuwa jeshi la Israel jana Ijumaa lilifanya shambulizi la anga katika mji wa Rafah na kuua watu wasiopungua sita. Zaidi ya Wapalestina milioni moja wamejihifadhi katika mji wa Rafah. Maafisa wa UN wanasisitiza tena umuhimu wa "kutokuwa na mashambulizi" katika jiji hilo.