Ndugu wa raia wa Japani waliotekwa na Korea Kaskazini wanasema wamepata uelewa wa Marekani

Ndugu wa raia wa Japani waliotekwa nyara na Korea Kaskazini wamerejea kutoka katika ziara yao nchini Marekani. Walisema waliweza kupata uelewa wa maafisa wa serikali ya Marekani na wabunge kuhusu kutatua suala la mateka.

Ndugu hao walitembelea Marekani kuanzia Jumatatu wiki hii kutafuta msaada wa Marekani wa kuwarejesha nchini Japani mateka wote waliosalia.

Kikundi hicho ni pamoja na Yokota Takuya, ambaye dada yake Megumi alitekwa mwaka 1977 akiwa na umri wa miaka 13 na Iizuka Koichiro ambaye mama yake Taguchi Yaeko alitekwa wakati yeye akiwa na umri wa mwaka mmoja.

Pia walitoa wito kwa serikali ya Japani kutoacha hitaji la kuwarejesha nyumbani mateka wote kwa pamoja.

Katika ziara yao jijini Washington, kikundi hicho kilikutana na maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya Marekani, ikiwa ni pamoja na Mira Rapp-Hooper wa Baraza la Usalama wa Taifa na Uzra Zeya, Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, Demokrasia na Haki za Binadamu, pamoja na wajumbe wa mabaraza yote ya bunge la Kongresi.

Mwezi Februari mwaka huu, kikundi hicho kiliamua kuwa hakitapinga Japani kuondoa vikwazo vyake kwa Korea Kaskazini ikiwa nchi hiyo itarejesha mateka wote wakati wazazi wao wakiwa hai.

Kikundi hicho kilisema kilielezea msimamo huu kwa upande wa Marekani na ukupata uelewa wao.

Jana Jumamosi Yokota aliwaambia wanahabari katika uwanja wa ndege wa Haneda jijini Tokyo kuwa watu wengi waliokutana nao walionyesha uelewa kuhusu machungu ya wanafamilia na kuwaambia kuwa Marekani ipo nao.

Pia alisema kikundi hicho kiliweza kuwasilisha ujumbe kwamba suala la mateka ni tatizo la haki za binadamu ambalo lina ukomo wa muda kwa ajili ya utatuzi.

Yokota alitoa wito kwa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kuamua vizuri kutatua suala hilo.