Timu ya soka ya wanaume ya Japani chini ya miaka 23 yashinda Kombe la Asia

Timu ya soka ya wanaume ya Japani imetwaa Kombe la Asia kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 23. Iliishinda Uzbekistan 1-0 katika mchezo wa fainali juzi Ijumaa na hivyo kulitwaa kombe hilo kwa mara ya pili.

Pande zote mbili zilishindwa kutengeneza nafasi nyingi, lakini mchezo huo ulichangamka katika dakika za majeruhi.

Katika dakika ya 91, Yamada Fuki aliyeingia kutoka benchi hatimaye alifunga bao. Goli lake lilionekana kuihakikishia ushindi Japani.

Lakini muda mfupi baadaye, mwamuzi aliamuru upigwe mkwaju wa penati. Mapitio ya picha ya video yalionyesha kuwa mchezaji wa Japani aliushika mpira kwenye eneo la penati.

Uzbekistani walipewa nafasi ya mwisho ya kusawazisha. Lakini kipa wa Japani Kokubo Leo Brian aliokoa, hivyo kuihakikishia Japani kulitwaa kombe hilo. Kokubo alisema baada ya mtanange huo kwamba “Tulifungwa na Uzbekistan miaka miwili iliyopita, hivyo timu yote ilinuwia kulipiza kisasi,” alisema Kokubo baada ya mchezo kumalizika. Nimefurahia kwamba tumetwaa kombe kwa ajili ya nchi yetu.”

Michuano hiyo pia hutumika kwa ajili ya kumsaka mwakilishi wa Asia katika mashindano ya Olimpiki ya Paris. Nchi hizo mbili Uzbekistani na Japani tayari zimeshajinyakulia nafasi mbili za kushiriki Olimpiki kufuatia kutinga nusu fainali ya Kombe la Asia.

Iraq pia ilijinyakulia tiketi kama hiyo kwa kuifunga Indonesia katika mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu. Indonesia sasa itaikabili Guinea mnamo Mei 9 katika mchezo wa kuisaka nafasi ya mwisho.

Japani itakuwa katika Kundi D kwenye Olimpiki. Itapambana na Paraguay, Mali na Israel. Uzbekistan imepangwa katika Kundi C lenye timu za Hispania, Misri na Jamhuri ya Dominica. Iraq ipo katika Kundi B pamoja na Argentina, Morocco na Ukraine.