ASEAN na nchi zingine tatu kuanzisha taasisi mpya ya ufadhili kwa ajili ya dharura

Mawaziri wa fedha na magavana wa benki kuu kutoka Japani, China, Korea Kusini na Mataifa ya Ushirikiano wa Nchi za Kusini-mashariki mwa Asia, ASEAN wamekubaliana kuanzisha taasisi mpya iliyoundwa kwa ajili ya kutoa fedha kwa wahusika itokeapo dharura kama vile majanga ya asili au magonjwa ya mlipuko.

Washiriki, akiwemo Waziri wa Fedha wa Japani Suzuki Shunichi na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Japani Himino Ryozo, walikutana jana Ijumaa jijini Tbilisi, nchini Georgia.

Wajumbe walikubaliana kwamba taasisi hiyo mpya itaanzishwa chini ya mradi wa Chiang Mai ulioanzishwa baada ya mgogoro wa kifedha wa Asia mwaka 1997.

Walisema taarifa za kina zitafanyiwa kazi hadi mwaka 2025.

Suzuki alisema katika mkutano na wanahabari baada ya mkutano wa wakuu hao kumalizika kuwa taasisi hiyo mpya itatoa usaidizi wa haraka katika jibizo la mishtuko ya nje, kama vile magonjwa ya milipuko na majanga ya asili.

Alielezea makubaliano hayo kama ukamilishaji mkubwa, akisema nchi za ASEAN, ambazo hukabiliwa na majanga ya asili, zina matumaini makubwa kwa taasisi hiyo mpya.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo ilisema hatari, kama vile kuongezeka kwa hali tete ya soko la fedha za kigeni, zinaweza kuathiri matarajio ya uchumi ya nchi hizo tatu na wanachama wa ASEAN katika muda mfupi.