China yarusha chombo cha uchunguzi kwenye upande wa mwezi ulio mbali zaidi

Maafisa wa shirika la anga za juu la China wanasema wamefanikiwa kurusha chombo cha uchunguzi kisichobeba rubani ili kukusanya sampuli kutoka upande wa mwezi ulio mbali zaidi.

Tangazo hilo lilikuja jana Ijumaa, muda mfupi baada ya chombo cha anga aina ya Chang'e-6 kurushwa kutoka eneo la kisiwa cha Hainan kusini mwa China.

Chombo hicho kimeundwa kuweza kurudi na mawe na sampuli zingine.

Ikiwa itafanikiwa, misheni hiyo itakuwa ya kwanza ya aina yake. Lakini wataalamu wanasema kuna changamoto kubwa.

Mwendelezo wa mawasiliano ya moja kwa moja na chombo hicho cha uchunguzi mwezini hayawezekani kwa sababu mawimbi ya redio kutoka Duniani hayaufikii upande wa mwezi ulio mbali zaidi na Dunia.

Maafisa hao wa China wanasema wanapanga kukusanya sampuli zenye thamani ya takribani kilo mbili na kurejesha uchunguzi huo Duniani siku 53 baada ya kurushwa kwa chombo hicho.

Utafiti wa anga za juu unazidi kuwa wa ushindani, huku nchi nyingi zikijiunga na nyanja inayoongozwa na Marekani kwa miaka mingi.