Mawaziri wa ulinzi wa Japani, Marekani, Australia na Ufilipino wakutana kukabiliana na China

Mawaziri wa ulinzi wa Japani, Marekani, Australia na Ufilipino wamekubaliana kuongeza ushirikiano katika jitihada za kukabiliana na ongezeko la uthubutu wa China.

Walikutana katika jimbo la Hawaii nchini Marekani juzi Alhamisi. Mawaziri hao wa ulinzi, Kihara Minoru wa Japani, Lloyd Austin wa Marekani, Richard Marles wa Australia na Gilberto Teodoro wa Ufilipino baadaye walizungumza na wanahabari kwenye mkutano wa pamoja.

Mawaziri hao wa ulinzi walibainisha wasiwasi wao mkubwa juu ya maendeleo kwenye Bahari za China Kusini na Mashariki, wakirejelea vizuizi vya mara kwa mara vya China juu ya uhuru wa kusafiri kwa meli za Ufilipino kwenye maji ya kimataifa.

Mawaziri hao pia walithibitisha kwamba nchi hizo nne zitaimarisha ushirikiano ili kufikia eneo huru na wazi la Indo-Pasifiki, kwa kufanya mafunzo mengi zaidi ya pamoja kufuatia awamu ya kwanza kama hiyo iliyofanyika mwezi uliopita.