Marekani yakiri shambulizi lake la anga nchini Syria lilimuua raia mmoja kimakosa

Jeshi la Marekani limeelezea masikitiko yake kufuatia shambulizi la anga lililofanywa mwaka jana nchini Syria likimlenga kiongozi mwandamizi wa kundi la Al Qaeda. Shambulizi hilo lilisababisha kifo cha raia mmoja.

Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani ilichapisha taarifa jana Alhamisi ikisema kwamba shambulizi la anga lililolenga kukabiliana na ugaidi lilitekelezwa kaskazini magharibi mwa Syria mwezi Mei mwaka jana na kumuua mwanamume mmoja.

Taarifa hiyo inasema uchunguzi wa jeshi hilo uliofanywa baadaye ulibaini kuwa wanajeshi wa Marekani walimtambua kimakosa kiongozi wa Al Qaeda aliyelengwa na raia mmoja aliyeitwa Lutfi Hasan Masto aliuawa.

Kamandi hiyo Kuu ya Marekani inasema inakiri na kusikitikia madhara yaliyofanywa kwa raia huyo. Imeahidi “kuendelea kutekeleza taratibu zenye ukamilifu na za hadhari za ulengaji na mashambulizi ili kupunguza madhara kwa raia.”

Jeshi la Marekani lilianzisha uchunguzi baada ya gazeti la Washington Post kuripoti mwezi Mei mwaka jana kuwa shambulizi la droni lililofanywa na nchi hiyo huenda pia lilipiga kimakosa eneo ambalo halikulengwa.