Uturuki yasitisha biashara na Israel kufuatia hali ya kibinadamu Gaza

Wizara ya Biashara ya Uturuki inasema nchi hiyo imesitisha biashara zote na Israel ikitaja kile ilichokiita kuwa janga la kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Tangazo hilo la jana Alhamisi linasema hatua hiyo itaendelea hadi Israel iruhusu msaada wa kutosha wa kibinadamu kupelekwa katika ukanda huo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Katz aliandika katika mitandao ya kijamii jana Alhamisi kuwa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alikuwa “anazuia bandari kutumiwa kwa uagizaji na usafirishaji nje ya nchi wa bidhaa za Israel.” Waziri huyo aliongeza kuwa, “Hivi ndivyo dikteta anavyokuwa.”

Katz alisema ameagiza afisa mwandamizi wa wizara ya mambo ya nje “kuanzisha mibadala ya biashara na Uturuki, akiangazia uzalishaji wa ndani ya nchi na uagizaji bidhaa kutoka nchi zingine.”

Takwimu kutoka ofisi kuu ya takwimu ya Israel zinaonyesha kuwa bidhaa zilizoagizwa na nchi hiyo mwaka 2023 zilikuwa za thamani ya dola bilioni 4.6, zikiwa za tano kwa ukubwa zaidi baada ya China, Marekani na mataifa mengine mawili.

Serikali ya Uturuki tangu mwezi Aprili mwaka huu imeweka vikwazo kwa bidhaa zinazosafirishwa kuelekea nchini Israel vikiathiri makundi 54 ya bidhaa ikiwa ni pamoja na chuma na saruji.