Hamas: Kiongozi wake anatathmini pendekezo la usitishaji vita katika ‘ari chanya’

Kundi la Hamas linasema kiongozi wake Ismail Haniyeh anatathmini pendekezo la usitishaji vita katika eneo la Gaza katika “ari chanya.”

Kupitia taarifa iliyotolewa katika mitandao ya kijamii jana Alhamisi, Hamas ilisema Haniyeh alizungumza na mkuu wa ujasusi wa Misri kwa njia ya simu.

Misri ni mpatanishi wa makubaliano kati ya Israel na Hamas juu ya usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza na kuachiliwa kwa mateka waliosalia wanaoshikiliwa katika ukanda huo.

Taarifa hiyo inasema Haniyeh aliihakikishia Misri kuwa ujumbe wa Hamas utaitembelea Misri haraka iwezekanavyo “ili kuhitimisha mazungumzo yanayoendelea.”

Vyombo vya habari vyenye makao yake Mashariki ya Kati vilikinuu chanzo cha habari cha Misri kikisema ujumbe wa Hamas utawasili mjini Cairo ndani ya siku mbili.

Hata hivyo, hatima ya mazungumzo hayo bado haijulikani. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anaonekana kuwa tayari kuendelea mbele na mashambulizi ya ardhini yaliyopangwa mjini Rafah.