China kurusha chombo kisichokuwa na rubani kuchunguza sehemu ya mbali ya mwezi

Leo Ijumaa, China itarusha chombo kisichokuwa na rubani mwezini ili kukusanya sampuli kutoka upande wa mwezi ambao kamwe hauonekani duniani.

Chombo hicho aina ya Chang'e-6 kimepangiwa kupaa kwenda upande wa mbali wa mwezi kutoka eneo la kurushia katika Jimbo la Hainan kusini mwa nchi hiyo.

Misheni ya "urejeshaji wa sampuli" inalenga kukusanya na kurudisha mawe na vielelezo vingine.

Afisa wa Mamlaka ya Taifa ya Anga za Juu ya China alisisitiza umuhimu wa misheni hiyo kwa wanahabari kwenye eneo la kurushia jana Alhamisi.

Afisa huyo alisema kwamba sampuli hizo zitasaidia wanadamu kuelewa zaidi asili ya mwezi.

Alisema wanatumai kuwa misheni hiyo itatoa thamani ya kisayansi sio tu kwa China bali pia kwa wanadamu wote.

Wataalam wanasema kituo cha mwisho kinaongeza kiwango cha ugumu kwenye misheni hiyo. Kuendelea kuwasiliana moja kwa moja na chombo hicho haiwezekani kwa sababu mawimbi ya redio kutoka duniani hayafikii upande wa mbali wa mwezi. Ikiwa itafanikiwa, misheni hiyo itakuwa ya kwanza ya aina yake kuwahi kutekelezwa.

Waangalizi wa mambo wanasema China inaonekana inalenga kuimarisha uwepo wake katika maendeleo ya anga, eneo linaloongozwa na Marekani kwa miaka mingi.