Kuporomoka kwa barabara kuu kwasababisha vifo vya watu wasiopungua 36 kusini mwa China

Kipande cha barabara kuu kimeporomoka jana Jumatano huko kusini mwa China, na kusababisha magari 23 kuanguka kwenye mteremko. Televisheni inayoendeshwa na serikali ya nchi hiyo, China Central inasema hadi sasa watu 36 wamethibitika kufariki dunia, na wengine 30 wamejeruhiwa.

Televisheni hiyo ilisema kipande cha barabara chenye urefu wa takribani mita 18 kwenye eneo la milima ya Meizhou, Jimbo la Guangdong, kilianguka mapema jana Jumatano.

Inasema magari 23 yaliangukia chini ya mteremko katika eneo ilipoporomoka barabara hiyo.

Nchini China, kipindi cha mapumziko ya siku tano ya Sikukuu ya Wafanyakazi au Mei Mosi kilianza jana Jumatano, na msongamano mkubwa wa magari kwenye barabara kuu umekuwa ukiongezeka.

Kumekuwepo na mfululizo wa mafuriko na kuporomoka kwa udongo kwenye Jimbo la Guangdong tangu mapema mwezi Aprili kutokana na mvua kubwa iliyovunja rekodi.

Baadhi ya vyombo vya habari vya China vimeripoti mvua kubwa imeendelea jirani na eneo la tukio.