Wadau wa masoko wanashuku kuwa serikali na BOJ ziliingilia kati soko

Kwenye soko la kubadilisha fedha za kigeni, sarafu ya yeni ya Japani ilipanda kwa kasi muda mfupi baada ya saa 11 alfajiri leo Alhamisi, kwa saa za nchi hiyo.

Wadau wa masoko wanashuku kuwa serikali ya Japani na Benki Kuu ya nchi hiyo BOJ huenda ziliingilia kati soko hilo.

Baada ya mkutano wa sera wa Benki Kuu ya Marekani, yeni ilipanda zaidi ya yeni nne hadi kiwango cha 153 dhidi ya dola.

Yeni ilipanda kiwango kama hicho Jumatatu iliyopita. Wadau wa masoko wanasema kuna uwezekano mkubwa kwamba serikali ya Japani na BOJ mara kwa mara zilifanya uingiliaji wa siri, na kufanya soko kuwa na wasiwasi.

Mamlaka za fedha za Japani hazijatoa tangazo rasmi kwa wakati huu.

Yeni imedhoofika leo Alhamisi asubuhi, kwa saa za Japani. Inauzwa kiwango cha karibu 156 dhidi ya dola kufikia saa 4 asubuhi. Vuta nikuvute inaendelea kati ya serikali ya Japani, BOJ na soko.