Polisi wakabiliana na waandamanaji kwenye kampasi nchini Marekani

Vyuo vikuu kote nchini Marekani vimeshuhudia maandamano ya kupinga mgogoro wa Gaza yakiwa vurugu zaidi. Polisi wa New York wamewakamata watu 300 kuanzia juzi Jumanne usiku hadi jana Jumatano asubuhi.

Chuo Kikuu cha Columbia kinajaribu kurejesha utulivu katika kampasi hiyo baada ya usiku wa machafuko. Makumi ya watu walikuwa wamejificha ndani ya jengo kabla polisi kuvamia. Waandamanaji wengine walipambana na maafisa hatua chache kutoka chuo cha City College jijini New York.

Meya wa Jiji la New York Eric Adams alifanya mkutano na wanahabari baada ya ukamataji huo. Alisema, “Hatuwezi kuruhusu yale yaliyokuwa maandamano ya amani kugeuka kuwa onyesho la vurugu lisilo na tija wala manufaa yoyote.”

Polisi pia waliitwa kwenye Chuo Kikuu cha California, Los Angeles, ambapo watu wanaoiunga mkono Palestina na wale wanaoiunga mkono Israel walikabiliana. Iliwachukua saa kadhaa kudhibiti vurugu hizo.

Mwanafunzi mmoja alisema watu walikuwa wakiwapiga wengine kwa kutumia magongo ya besiboli na fimbo na kurusha “chochote walichoweza kukirusha.” Alisema ilichukua muda kwa polisi kufika kwenye eneo la tukio.

Utawala wa Chuo Kikuu cha California ulisema mbinu za baadhi ya waandamanaji zimekuwa za “kushtusha na aibu.” Wameahirisha madarasa.