Kishida asisitiza ‘utaratibu wa uchumi ulio huru na wa haki’ katika mkutano wa OECD

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio jana Alhamisi alihutubia mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, OECD jijini Paris nchini Ufaransa.

Japani ni mwenyekiti wa mkutano huo ambapo mwaka huu wa 2024 inatimia miaka 60 tangu ilipojiunga na OECD.

Waziri huyo mkuu wa Japani alibainisha kuwa ni vigumu zaidi kwa nchi kuwa na makubaliano kwani jumuiya ya kimataifa imekuwa na mitazamo tofauti sana kutokana na migogoro mingi na kuibuka kwa nchi zinazochipukia kiuchumi.

Hata hivyo alisema kwamba, mabadiliko ya nyakati na kukabiliana na matatizo kunaweza kuwa fursa ya kuboresha zaidi maisha ya watu. Alielezea nia yake ya kuendelea kushirikiana na nchi zingine wanachama wa OECD, akibainisha kuwa Japani inafanya kazi kuanzisha kichocheo kipya cha ukuaji kwa kutatua masuala kwa kutumia ujuzi na maarifa ya shirika hilo.

Kishida alisema kuwa Japani itafanya kazi na nchi zenye mtazamo sawa katika kufikia uchumi thabiti na kuimarisha usalama wa kiuchumi.

Aliongeza kwamba Japani, miongoni mwa nchi chache wanachama wa OECD barani Asia, imedhamiria kuwa daraja la kuunganisha maeneo na kusaidia shirika hilo kuongoza uchumi wa dunia.