Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani alizuru nchi tatu za Afrika

Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani Kamikawa Yoko alizuru nchi za Madagascar, Cote d’Ivore na Nigeria katika ziara yake ya siku tano katika nchi zinazochipukia kiuchumi barani Afrika. Ziara hiyo ilikamilika juzi Jumatano.

Kamikawa ni Waziri wa Mambo ya Nje wa kwanza wa Japani kuzuru Madagascar ambayo ni nchi ya kisiwa katika Bahari ya Hindi. Alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar Rasata Rafaravavitafika na kuthibitisha kuwa watashirikiana katika juhudi za kufikia eneo huru na la wazi la Indo-Pasifiki linalozingatia utawala wa sheria.

Wakati wa ziara yake nchini Nigeria, ambayo ni nchi yenye utajiri mkubwa wa maliasili, Kamikawa na Waziri wa Mambo ya Nje wa wa nchi hiyo Yusuf Tuggar walikubaliana kuwa watakuza ushirikiano wa kiuchumi kama vile utoaji misaada kwa kampuni zinazochipukia nchini Nigeria.

Ziara ya Kamikawa kwenye mataifa ya Afrika na Asia ni sehemu ya juhudi za serikali ya Japani za kuongeza ushirikiano na nchi zinazochipukia kiuchumi na zile zinazoendelea, ambazo kwa pamoja zinajulikana kama nchi za Kusini mwa Dunia, yaani Global South.

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio anatarajiwa kuzuru Brazil na Paraguay zilizopo Amerika Kusini baada ya mkutano wa OECD.