Ripoti: Biden asema Japani ni ‘nchi inayowachukia wageni’ kwenye tukio la kampeni ya uchaguzi

Ripoti za vyombo ya habari zinasema kuwa Rais Joe Biden wa Marekani ameshutumu kwamba shida za kiuchumi zinazoikabili Japani zimetokana na chuki ya nchi hiyo dhidi ya wageni huku akidai kwamba uchumi wa Marekani unakua kwa sababu ya kuwakubali wahamiaji.

Imeripotiwa kwamba Biden alitoa maoni hayo kwenye tukio la kuchangisha fedha kwa ajili ya kampeni yake ya kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa mwaka huu lililofanyika jijini Washington jana Jumatano.

Shirika la habari la Reuters lilimnukuu Biden akisema moja ya sababu ya uchumi wa Marekani kukua ni kuwakubali wageni.

Biden aliendelea kusema kuwa, “Kwa nini China imekwama vibaya kiuchumi, kwa nini Japani inakabiliwa na matatizo, kwa nini Urusi, India, ni kwa sababu ya kuwachukia wageni. Hawawataki wahamiaji. Wahamiaji ndio wanaotufanya kuwa imara.”

Chombo cha habari cha Marekani, Bloomberg pia kimeripoti juu ya maoni ya Biden. Kilisema kwamba Biden ameunganisha matatizo ya kiuchumi ya China kuwa yametokana na kutokuwa tayari kuwakubali wageni hapo kabla, wakati huu ameiongeza Urusi na mshirika wake wa muda mrefu, Japani.

Bloomberg imeainisha kwamba Biden alimpokea Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio kwa mkutano wa viongozi wakuu na hafla ya kitaifa jijini Washington, majuma matatu yaliyopita.

Kilibainisha kwamba ukosoaji wa Biden na ukweli kwamba Japani ilitajwa sambamba na mataifa mawili makubwa asimu ya Marekani kunaweza kuzua ukosoaji nchini Japani.