Nchi 49 na Umoja wa Ulaya zatafuta utaratibu mpya wa kufuatilia vikwazo vya Korea Kaskazini

Nchi 49 na Umoja wa Ulaya, EU zimetoa taarifa ya pamoja kutaka kuwepo kwa utaratibu mpya wa kufuatilia vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini.

Jopo la wataalam wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lililopewa jukumu hilo lilivunjwa mnamo Aprili 30 baada ya Urusi kupiga kura ya turufu dhidi ya azimio la kuongeza muda wa jopo hilo. Jopo hilo lilitoa ripoti na uchambuzi kuhusu jinsi Korea Kaskazini imekuwa ikikwepa vikwazo na kuendelea na mipango yake ya uendelezaji wa nyuklia na makombora.

Balozi wa Marekani katika UN Linda Thomas-Greenfield alisoma taarifa ya pamoja katika makao makuu ya UN jijini New York jana Jumatano.

Alisema kura ya turufu ya Urusi "iliyanyima Mataifa Wanachama wa UN taarifa muhimu na mwongozo wa kutekeleza hatua zilizopitishwa na baraza hilo."

Pia aliitaka Korea Kaskazini kuachana na mipango yake ya silaha za maangamizi ya halaiki na makombora ya balistiki.

Balozi huyo alisema, "Kwa kuzingatia umuhimu kwa Nchi Wanachama wote kuzingatia maazimio husika ya Baraza la Usalama, na kwa kuzingatia kumalizika muda kwa jopo hilo, lazima sasa tufikirie jinsi ya kuendelea kupata aina hii ya uchambuzi huru na usio na upendeleo."