Blinken: Marekani haiwezi kuunga mkono mashambulizi makubwa ya Israel huko Rafah

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken anasema nchi hiyo haiwezi kuunga mkono operesheni kubwa ya Israel katika mji wa Rafah kusini mwa Gaza bila kuwepo kwa mpango unaofaa wa kuwalinda raia.

Blinken amezungumza hayo baada ya mkutano na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu nchini Israel jana Jumatano.

Blinken aliwaambia wanahabari kwamba serikali ya Israel haijawasilisha mpango unaofaa wa kibinabamu. Ameongeza kuwa kuna njia zingine za kukabiliana na Hamas ambazo hazihusishi operesheni kubwa mjini Rafah.

Netanyahu awali alisema ataendelea na mashambulizi mjini Rafah yawepo makubaliano au la.

Blinken amesema kuna makubaliano kati ya Marekani na Israel kuwa endapo makubaliano ya kusitisha vita na kuachia mateka yatafikiwa, “tutatafuta njia za kuendeleza kwenye hilo na kuwa na kitu ambacho ni endelevu muda hadi muda.”

Amesisitiza wito wake kwa Hamas wa kukubali makubaliano ya usitishaji vita.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Karine Jean-Pierre jana Jumatano aliwaambia wanahabari kwamba usititishaji vita kama sehemu ya makubaliano ya mateka unapaswa “kutokea mara moja.”

Amesema Hamas bado hawajajibu.