Uingereza yawashikilia wahamiaji wasio na vibali kabla ya kuwahamishia Rwanda

Serikali ya Uingereza imetangaza kwamba mamlaka za nchi hiyo zimeanza kuwakamata wahamiaji wasio na vibali ili kujiandaa kuwahamishia Rwanda.

Hatua hiyo ya jana Jumatano imekuja baada ya Sheria ya Usalama ya Rwanda kupitishwa mwezi uliopita. Sheria hiyo imetungwa kwa lengo la kuwahamishia nchini Rwanda watu wanaotafuta hifadhi walioingia Uingereza bila ruhusa.

Serikali hiyo imebainisha kuwa hatua za kukabiliana na wahamiaji wanaoingia Uingereza kinyume cha sheria kisha kuomba hadhi ya ukimbizi, zimekuwa mzigo mkubwa wa kifedha.

Serikali ya Uingereza pia jana Jumatano ilitoa picha za maafisa wa uhamiaji wakivamia nyumba za watu binafsi wanaoaminika kuwa tayari kuhamishiwa Rwanda. Maafisa walionekana wakiwatia pingu na kuwaweka kwenye magari.

Idadi ya waliokamatwa, na mahala walipokamatiwa, bado haijafahamika. Lakini serikali inasema uvamizi umefanyika kote nchini Uingereza.

Makundi ya kuwasaidia wahamiaji wanaotafuta hifadhi yameshutumu mpango huo wa uhamishaji, wakisema unakiuka haki za binadamu.

Utawala wa Waziri Mkuu Rishi Sunak unaonekana kuwa tayari kushuhudia ndege ya kwanza ya uhamishaji ikiondoka kufikia mwezi Julai. Ilitangaza mipango ya kufanya uvamizi zaidi katika kipindi cha majuma kadhaa yajayo na kutuma ndege nchini Rwanda katika kipindi cha majuma tisa hadi kumi na moja yajayo.