Watu zaidi ya 4,600 bado wanaishi katika makazi ya muda ikiwa ni miezi minne baada ya tetemeko la Japani

Mei Mosi inatimia miezi minne tangu tetemeko kubwa la ardhi litokee katika Rasi ya Noto na maeneo jirani katikati mwa Japani, wakati watu zaidi ya 4,600 bado wapo kwenye makazi ya muda. Nyumba za muda zinajengwa katika mkoa wa Ishikawa.

Idadi ya vifo vilivyothibitishwa kutokana na tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.6 katika kipimo cha Richter ni watu 245 katika mkoa wa Ishikawa na watatu hawajulikani walipo.

Katika mkoa huo, nyumba 78,568 zimeharibiwa na tetemeko hilo. Kati ya hizo, asilimia zaidi ya 10 ama nyumba 8,142 zimebomoka kabisa.

Hadi kufikia mwezi Aprili, takribani nyumba za muda 3,300 zilikuwa tayari zimejengwa, ambapo ni asilimia zaidi ya 50 ya kile mkoa huo inaamini inahitaji.

Watu wengi hawawezi kurejea nyumbani katika miji ya Suzu na Wajima kutokana na huduma ya maji kutorejea katika nyumba takribani 3,780.

Mkoa wa Ishikawa unahamasisha ujenzi wa nyumba za muda kwa lengo la kuwawezesha wale wote wanaopenda kuhamia katika nyumba kama hizo kufikia Agosti. Isipokuwa baadhi ya maeneo, mkoa huo unatumai kutatua suala la kukatika kwa maji katika mwezi huu wa Mei, ambapo wanapambana na tatizo ili kusaidia watu walioathirika na tetemeko la ardhi kurejea katika maisha yao ya kawaida.