Polisi wa New York waingia Chuo Kikuu cha Columbia kuwaondoa waandamanaji

Polisi katika jiji la New York nchini Marekani wamevamia Chuo Kikuu cha Columbia ili kuwaondoa waandamanaji wanaopinga mashambulizi ya Israel katika eneo la Gaza.

Jana Jumanne usiku, maafisa wengi wa polisi walipanda na kuingia kwenye jengo hilo kupitia dirishani.

Kabla ya kuingia chuoni hapo, polisi waliwaambia waandishi wa habari kwamba maandamano yaliyokuwa ya amani yalitumiwa vibaya na wachochezi kutoka nje. Walionyesha utayari wao wa kushirikiana na chuo hicho ikiwa kitaomba msaada.

Wanafunzi wameweka mahema kwenye kampasi ya chuo hicho kupinga mashambulizi ya Israel. Baadhi ya waandamanaji waliteka jengo jana Jumanne, siku moja baada ya chuo hicho kutangaza kuwa kitawasimamisha masomo wanafunzi ambao watakiuka muda wa mwisho uliowekwa wa kuondoka kwenye jengo hilo.

Mnamo Aprili 18, polisi waliwakamata waandamanaji zaidi ya 100 katika Chuo Kikuu cha Columbia waliokataa kutawanyika. Tangu wakati huo, maandamano yameenea kwenye vyuo vikuu vingine kote nchini Marekani.