Wachambuzi wasema Japani huenda ilichukua hatua za kununua yeni

Wachambuzi wanaamini serikali ya Japani na Benki Kuu ya nchi hiyo BOJ huenda zilichukua hatua ya kununua yeni yenye thamani ya takribani trilioni tano ama takribani dola bilioni 32 ili kuzuia sarafu hiyo ya Japani isiporomoke kwa kasi.

Waangalizi wa masoko wanashuku kuwa serikali ya Japani na BOJ zilichukua hatua hizo bila kutangaza, ambapo yeni ilirejea kwa kasi kubwa mara kadhaa juzi Jumatatu. Kwa mfano, sarafu hiyo ilipanda hadi kufikia kiwango cha yeni 154 dhidi ya dola baada ya kuporomoka hadi kufikia yeni 160 dhidi ya dola.

Naibu Waziri wa Fedha wa Masuala ya Kimataifa Kanda Masato mara kwa mara amekuwa akikanusha kuzungumzia suala hilo. Takwimu ambazo zitatolewa na Wizara ya Fedha mwishoni mwa mwezi Mei zitaonyesha iwapo hatua zozote zilichukuliwa.