Kishida aondoka kuelekea Ufaransa, Brazil na Paraguay kwa ziara ya siku sita

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio leo Jumatano ameanza ziara ya siku sita katika nchi za Ufaransa, Brazil na Paraguay.

Akiwa nchini Ufaransa, Kishida atahudhuria mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo. Japani itakuwa mwenyekiti wa mkutano huo.

Kishida anapanga kutoa hotuba katika mkutano huo. Waziri Mkuu huyo wa Japani atasisitizia umuhimu wa kudumisha na kuimarisha utaratibu wa kiuchumi ulio huru na wa haki.

Kishida anadhamiria kutangaza kuanzishwa kwa mfumo wa kimataifa ili kujadili ukuzaji wa matumizi ya teknolojia ya Akili Kompyuta zalishi na kutengeneza sheria za kutatua changamoto zake.

Pia anatarajiwa kuonyesha utayari wa Japani wa kukabiliana na changamoto zingine za kidunia, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi.

Kishida atafanya mazungumzo na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron katika chakula cha mchana.

Kisha waziri mkuu huyo wa Japani atatembelea Brazil ambayo ni rais wa zamu wa Kundi la Mataifa 20 yaliyostawi zaidi kiuchumi, G20 na kisha nchini Paraguay kwa ajili ya mazungumzo ya viongozi wakuu.