Netanyahu aapa kuendelea na mashambulizi mjini Rafah

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasema ataendelea na mashambulizi katika mji wa Rafah uliopo kusini mwa Gaza ikiwa makubaliano yatafikiwa ama yasipofikiwa.

Netanyahu ametoa kauli hiyo jana Jumanne wakati wa mkutano na ndugu wa mateka na familia zilizoondokewa na wapendwa wao.

Alisema, “Wazo kwamba tutasitisha vita kabla ya kufanikiwa malengo yetu yote hilo halipo.”

Waziri mkuu huyo alielezea dhamira yake ya “kuingia Rafah” na “kuangamiza vikosi vya Hamas” ili “kupata ushindi kamili.”

Jeshi la Israel linajiandaa kwa ajili ya mashambulizi ya ardhini katika mji wa Rafah. Lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Israel Katz Jumamosi iliyopita alisema kwamba nchi hiyo inaweza kusitisha mpango huo ikiwa itafikia makubaliano ya mateka na Hamas.

Maoni yake yalileta upinzani mkali kutoka kwa wanachama wa mrengo wa kulia katika serikali ya Israel. Waangalizi wa mambo wanagusia kuwa maoni hayo yalimpelekea Netanyahu kuonyesha upinzani wa wazi.

Televisheni ya Al Jazeera yenye makao yake nchini Qatar ilimnukuu mchambuzi wa kisiasa wa Palestina akisema kwamba maoni ya Netanyahu ya hivi karibuni yanatatiza mazungumzo yote ya kusitisha mapigano.