Mkutano wa G7 wapitisha taarifa inayojumuisha kuondoa nishati ya makaa ya mawe kufikia mwanzoni mwa miaka ya 2030

Mawaziri wa Nishati kutoka Kundi la Nchi Saba zilizostawi zaidi kiviwanda, G7 walimaliza mazungumzo ya siku mbili jijini Turin nchini Italia jana Jumanne. Mkutano huo ulifuatia mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi wa COP28 wa mwaka jana.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo inasema kuwa nchi za G7 zitasitisha matumizi ya makaa ya mawe katika uzalishaji wa umeme ifikapo katikati ya miaka ya 2030, "au kwa muda unaoendana na kikomo kilichowekwa cha ongezeko la nyuzi joto 1.5 za Selisiasi kuweza kufikiwa, sambamba na hewa chafuzi inayozalishwa na nchi hizo kutozidi ile inayoondolewa.”

Taarifa hiyo pia inatoa wito kwa nchi zingine kuwasilisha malengo yao mapya ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi kwa mwaka 2030 na kuendelea, ifikapo mapema mwaka ujao.

Pia inasema kuwa nchi za G7 zinalenga kuongeza mara tatu uwezo wa kimataifa wa kuzalisha nishati mbadala ifikapo mwaka 2030. Zinaweka lengo la kuongeza hifadhi ya nishati zaidi ya mara sita hadi gigawati 1,500 kutoka viwango vya sasa kupitia betri na njia zingine.

Taarifa hiyo pia inasema nchi za G7 zitaongeza ushirikiano katika kuunga mkono nchi zinazoendelea barani Afrika na maeneo mengine kwa ajili ya hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.