Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani azisihi Israel na Hamas kukubali kusitisha vita

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amejaribu tena kuwaleta wajumbe wa Israel na Hamas kwenye meza ya majadiliano. Alikutana na wanachama wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba jana Jumatatu mjini Riyadh nchini Saudi Arabia.

Blinken aliwaambia viongozi wa mataifa ya Ghuba na Mamlaka ya Palestina kuwa ameshuhudia “hatua kiasi ikipigwa” katika hali ya kibinadamu katika eneo la Gaza. Hata hivyo, alisema suluhisho la “haki zaidi” litakuwa kusitisha mapigano na kuwaleta nyumbani mateka wanaoshikiliwa na Hamas.

Blinken anaitaka Israel kuchukua hatua madhubuti ili kuwalinda raia katika eneo la Gaza. Anawataka viongozi wa Hamas kukubali kile anachokiita pendekezo la “ukarimu usiokuwa wa kawaida.” Wapatanishi hawajaweka wazi pendekezo la hivi karibuni la usitishaji vita la Israel, lakini ripoti za vyombo vya habari zinaashiria kuwa Israel iko tayari kujadili usitishaji wa mgogoro huo kwa mabadilishano ya kuachiliwa kwa mateka. Blinken alisema, “Kitu pekee kinachosimama kati ya watu wa Gaza na usitishaji vita ni Hamas.”

Ripoti pia zinasema wapatanishi wa Hamas wako mjini Cairo nchini Misri kukutana na wapatanishi kutoka Misri na Qatar. Ripoti zinanukuu vyanzo vya habari vya Israel vikisema wajumbe wao wataelekea huko leo Jumanne.