Wabunge wa upinzani nchini Korea Kusini watembelea visiwa vya Takeshima vyenye mzozo

Chama kikuu cha upinzani nchini Korea Kusini kinasema wabunge wake na watu wengine wamefika kwenye visiwa vya Takeshima kwenye Bahari ya Japani.

Korea Kusini inavidhibiti. Japani inadai kuvimiliki na inasema Korea Kusini ilivitwaa kinyume cha sheria.

Tawi la kikanda la Chama cha Democratic linasema watu 17, wakiwemo wabunge watatu, waliwasili visiwani humo jana Jumanne. Korea Kusini inaviita visiwa hivyo kwa jina la Dokdo.

Kipande cha picha ya video kilichotumwa kwenye YouTube kinaonyesha wabunge wakiimba pamoja na bango linalosema, "Dokdo ni eneo letu."

Wizara ya mambo ya nje ya Japani ilituma malalamiko katika ubalozi wa Korea Kusini jijini Tokyo kuhusu ziara ya wabunge hao katika Visiwa vya Takeshima.

Ubalozi wa Japani jijini Seoul, pia ulituma malalamiko kama hayo kwenye wizara ya mambo ya nje ya Korea Kusini.