Timu ya soka ya umri wa chini ya miaka 23 ya Japani yafuzu Michezo ya Olimpiki ya Paris

Timu ya soka ya umri wa chini ya miaka 23 ya Japani imefuzu kwa Michezo ya Olimpiki ya Paris baada ya kupata ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Iraq katika mchuano wa nusu fainali wa mashindano ya mwisho ya kufuzu barani Asia.

Japani ilichukua uongozi wa mapema katika mechi hiyo iliyosakatwa jana Jumatatu nchini Qatar. Katika dakika ya 28, mshambulizi Hosoya Mao alipokea pasi ndefu na kwa uweledi akafunga goli la kwanza.

Goli la pili la Japani lilifungwa dakika ya 42 pale mchezaji Araki Ryotaro alipotikisa wavu baada ya mfululizo wa pasi fupi na za haraka.

Weledi wa mlinda mlango Kokubo Leo Brian kupangua mikwaju ya Iraq uliizuia kutia bao kimiani na Japani ilishinda mechi hiyo bila kufungwa goli.

Japani imefuzu Michezo ya Olimpiki kwani timu tatu za kwanza katika mashindano ya kufuzu barani Asia zinafuzu moja kwa moja.

Michezo ya Olimpiki ya Paris itakuwa ya nane mfululizo kwa timu ya wanaume ya Japani kushiriki tangu Michezo ya Atlanta mnamo mwaka 1996.