Marekani yathibitisha vitengo 5 vya Israel vilifanya ukiukaji wa haki za binadamu kabla ya Oktoba 7

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inasema imethibitisha kuwa vitengo vitano vya vikosi vya usalama vya Israel vilifanya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu kabla ya Oktoba mwaka jana, wakati mgogoro na Hamas ulipoanza.

Naibu msemaji wa wizara hiyo Vedant Patel aliwaambia wanahabari jana Jumatatu kuwa kati ya matukio hayo hakuna lililofanyika ndani ya eneo la Gaza. Aliongezea kuwa vinne miongoni mwa “vitengo hivyo vimerekebisha kikamilifu” ukiukaji huo.

Patel hakutoa taarifa yoyote mahususi kuhusiana na ukiukaji huo. Ila vyombo vya Habari vya Marekani vimeripoti kuwa vitengo vya Israel viliwatesa na kuwanyanyasa Wapalestina kwenye eneo la Ukingo wa Magharibi linalodhibitiwa na Israel.

Sheria ya Marekani inaizuia nchi hiyo kutoa msaada wa kijeshi kwa vitengo vya usalama vya kigeni, pale ambapo kuna taarifa za kuaminika zinazovihusisha na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Kabla ya mkutano wa Patel na wanahabari, vyombo vya habari vya nchi hiyo viliripoti kuwa Marekani inaweza kusitisha msaada wa kijeshi kwa vitengo vya Vikosi vya Ulinzi vya Israel. Ripoti hiyo iliibua majibu makali kutoka kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Sheria ya Marekani inaruhusu jambo la kipekee. Msaada wa kijeshi unaweza kutolewa, iwapo Waziri wa Mambo ya Nje atabaini kuwa vitengo vya usalama vilivyohusika vinachukuliwa hatua stahiki na serikali husika ili kuwafikisha wahusika mbele ya sheria.