Majadiliano ya mwisho juu ya makubaliano ya janga yaanza makao makuu ya WHO

Mataifa wanachama wa Shirika la Afya Duniani, WHO yameanza tena majadiliano yanayolenga kukamilisha makubaliano ya janga yaliyojikita kwenye mafunzo yaliyotokana na janga la virusi vya korona.

Mataifa hayo yalianza majadiliano hayo miaka miwili iliyopita.

Mataifa wanachama yanalenga makubaliano hayo ya janga kuidhinishwa wakati wa Baraza Kuu la WHO mwezi Mei mwaka huu.

Mkutano wa mwisho katika mfululizo wa mikutano juu ya makubaliano hayo ulianza faraghani jana Jumatatu katika makao makuu ya WHO mjini Geneva nchini Uswizi.

Rasimu ya makubaliano, ambayo ilitolewa mapema, inatoa wito kwa kila upande kuendeleza na kila baada ya muda fulani kuifanya kuwa ya kisasa mipango ya kitaifa ya kina ya uzuiaji wa majanga na uangalizi wa afya ya umma.

Pia inasema kwamba kila upande utakusanya rasilimali za kifedha za nyongeza ili kusaidia mataifa yanayoendelea.

Rasimu hiyo inakusudia kuhamasisha uhamishaji wa teknolojia na ujuzi ili chanjo na dawa ziweze kuzalishwa katika mataifa yanayoendelea.

Inahimiza taasisi za utafiti na za maendeleo na watengenezaji bidhaa kusamehe au kupunguza mirabaha katika matumizi ya teknolojia kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa za afya zinazohusiana na majanga wakati wa janga.

Vyanzo vyenye uelewa vinasema mataifa yanayoendelea yanataka wamiliki wa hataza husika kusamehe mirabaha lakini mataifa yaliyoendelea yana mashaka kuhusiana na athari ambayo hatua hiyo inaweza kuwa nayo kwa kampuni zao za kutengeneza dawa.

Bado haijabainika ikiwa pande hizo mbili zinaweza kufikia makubaliano kabla ya kumalizika kwa mkutano wa mwisho Mei 10.