Volkano yalipuka Indonesia

Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini Japani inasema kuwa hakuna hatari ya kutokea kwa tsunami nchini humo kufuatia mlipuko wa volkano nchini Indonesia.

Maafisa wa mamlaka hiyo wanasema kuwa Mlima Ruang uliopo katika jimbo la Sulawesi Kaskazini ulilipuka mapema leo Jumanne.

Wanasema moshi ulionekana ukifuka kwenye volkano hiyo kwa kiasi cha mita 19,000 kuelekea juu. Maafisa hao wamekuwa wakifuatilia mabadiliko ya mawimbi na masuala mengine yaliyosababishwa na mlipuko huo. Lakini wanasema hakuna mabadiliko makubwa katika viwango vya mawimbi ndani na maeneo yaliyo jirani na Japani.

Mlima Ruang awali ulilipuka Aprili 17 mwaka huu na kulazimisha wakazi wapatao 800 kukimbilia kisiwa kingine.

Mamlaka nchini Indonesia zinatoa wito kwa watu waliopo karibu na volkano hiyo kuhama mara moja baada ya mlipuko huo wa leo Jumanne. Pia zimewaambia wakazi wa kisiwa jirani kuchukua tahadhari dhidi ya tsunami inayoweza kutokea.