Mawaziri wa Nishati wa G7 kuidhinisha taarifa inayoelezea kwa muhtasari hatua za kupunguza gesi chafuzi

Mawaziri wa Tabianchi, Nishati na Mazingira kutoka Kundi la Nchi Saba zilizostawi zaidi kiviwanda, G7 wanatarajiwa kuidhinisha taarifa inayoelezea kwa muhtasari hatua za kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.

Mawaziri hao walianza mazungumzo ya siku mbili jijini Turin nchini Italia jana Jumatatu.

Kulingana na rasimu ya taarifa hiyo, nchi za G7 zinapanga kuzisihi nchi zingine kuwasilisha malengo yao mapya ya upunguzaji wa gesi chafuzi kufikia mwaka 2030 na baadaye kufikia mwaka ujao ikiwa ni mapema zaidi.

Taarifa hiyo inatoa wito wa kuondoa kwa awamu mitambo inayoendeshwa kwa makaa ya mawe ambayo haina hatua za kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi kufikia nusu ya kwanza ya miaka ya 2030, au kulingana na lengo la kupunguza kupanda kwa halijoto duniani hadi nyuzi 1.5 za Selisiasi juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda.

Ili kuongeza mara tatu uwezo wa nishati mbadala kufikia mwaka 2030, taarifa hiyo inatoa wito wa kuongeza hifadhi ya nishati kwenye sekta ya nishati kupitia betri za kutunzia nishati na njia zingine hadi gigawati 1,500. Hiyo ni mara sita zaidi ya viwango vya sasa.

Taarifa hiyo inasema nchi za G7 zinapanga kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi kutoka kwenye magari kwa njia mbalimbali na kuongeza miundombinu ya kuchajia magari ya umeme.

Pia zina mpango wa kutumia njia mbalimbali kukusanya data kuhusiana na taka za plastiki baharini.

Taarifa hiyo inatarajiwa kuidhinishwa leo Jumanne.