Ndugu wa mateka waelekea Marekani kuomba msaada

Ndugu wawili wa raia wa Japani waliotekwa nyara na Korea Kaskazini wameondoka nchini humo kuelekea Marekani kuomba msaada kutoka kwa maafisa wa Marekani kwa ajili ya kusuluhisha suala hilo mapema.

Ndugu hao ni Yokota Takuya, anayeongoza kundi la familia za waliotekwa nyara, na Iizuka Koichiro.

Yokota ni mdogo wa kiume wa Yokota Megumi, ambaye alitekwa nyara na mawakala wa Korea Kaskazini akiwa na umri wa miaka 13.

Mama yake Iizuka, Taguchi Yaeko alitekwa nyara na Korea Kaskazini wakati Iizuka alipokuwa na umri wa mwaka mmoja.

Wawili hao wanapanga kukutana na maafisa wa serikali na wabunge wa mabaraza yote mawili ya Bunge la Marekani kabla ya kurejea Japani siku ya Jumamosi.

Mnamo mwezi Februari, kundi la familia za waliotekwa nyara liliandaa mpango kazi ambao unasema hawatapinga serikali ya Japani kuondoa vikwazo kwa Korea Kaskazini ikiwa mateka wote waliosalia watarejeshwa ingali wazazi wao wakiwa hai.

Kundi hilo liliiasa vikali serikali ya Japani kuchukua hatua na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kufanya uamuzi.

Serikali ya Japani inasema raia wapatao 17 walitekwa nyara na mawakala wa Korea Kaskazini katika miaka ya 1970 na 1980. Watu watano walirejeshwa mwaka 2002, lakini wengine 12 bado hawajulikani waliko.