Biden, Netanyahu wajadili usitishaji mapigano Gaza na uachiliwaji wa mateka

Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wamejadili mazungumzo yanayoendelea kuhusu kuachiliwa kwa mateka na kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza wakati wa mazungumzo yao kwa njia ya simu.

Jana Jumapili, Ikulu ya Marekani ilitangaza kwamba viongozi hao wawili walipitia mazungumzo kati ya Israel na kundi la Hamas katika mazungumzo kwa njia ya simu mapema siku hiyo.

Ikulu ya Marekani ilisema katika taarifa kwamba Biden na Netanyahu "pia walijadili ongezeko la utoaji wa msaada wa kibinadamu huko Gaza ikiwa ni pamoja na kufanya maandalizi ya kufungua vivuko vipya vya mipaka ya kaskazini kuanzia wiki hii."

Biden alisisitiza juu ya "uhitaji wa hatua hiyo kuwa endelevu na kuimarishwa."

Rais huyo pia alisisitiza msimamo wake wa wazi wakati jeshi la Israel likiidhinisha mipango ya kuendeleza vita huko Gaza. Hatua hiyo inaaminika kuwa sehemu ya maandalizi ya mashambulizi ya ardhini katika mji wa kusini wa Rafah.

Biden ameelezea mara kwa mara wasiwasi wake mkubwa juu ya uwezekano wa operesheni ya ardhini ya Israel huko Rafah.

Anaaminika kuwasilisha wasiwasi huo kwa mshirika wake Israel wakati wa mazungumzo hayo.