Blinken aelekea Mashariki ya Kati kujadili usitishaji vita Gaza na uachiliwaji wa mateka

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ameondoka nchini humo kuelekea Mashariki ya Kati. Wizara hiyo inasema anapanga kuzungumza na “washirika wa kikanda” kuhusu juhudi zinazoendelea za kufanikisha usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza na kufanikisha uachiliwaji wa mateka wanaoshikiliwa huko.

Blinken ameondoka kwa ndege kutoka katika kambi ya jeshi la anga iliyopo viungani mwa jiji la Washington jana Jumapili. Atakwenda Saudi Arabia, Jordan na Israel hadi keshokutwa Jumatano.

Msemaji wa Usalama wa Taifa katika Ikulu ya Marekani John Kirby aliiambia ABC News kwamba Hamas haijakataa kabisa makubaliano ya mateka. Amesema kundi hilo linazingatia pendekezo lililowasilishwa na Israel.

Kirby amesema mapigano Gaza yatasitishwa kwa majuma sita ikiwa pendekezo hilo litakubaliwa. Ameongeza kuwa Marekani inatumai “jambo la kudumu zaidi” litakuwepo wakati usitishaji wa vita kwa muda utakapomalizika.