Chama kikuu cha upinzani nchini Japani CDP chashinda katika chaguzi ndogo 3

Chaguzi ndogo tatu za Baraza la Chini la Bunge zilifanyika nchini Japani jana Jumapili. Wagombea kutoka Chama kikuu cha upinzani cha Constitutional Democratic, CDP wameshinda viti vyote vitatu. Matokeo hayo yanatarajiwa kuathiri usimamizi wa serikali inayoongozwa na Waziri Mkuu Kishida Fumio.

Chaguzi hizo ndogo zilifanyika katika majimbo ya Tokyo na mikoa ya Shimane na Nagasaki.

Katika eneo namba 1 la Mkoa wa Shimane, mgombea kutoka chama cha upinzani cha CDP alikishinda chama tawala cha Liberal Democratic, LDP.

Uchaguzi katika eneo namba 15 la jijini Tokyo ulifanyika baada ya aliyekuwa naibu waziri wa sheria wa serikali kujiuzulu kwa madai ya kununua kura. Mgombea kutoka chama cha CDP ameshinda katika uchaguzi huo. LDP haikuweka mgombea katika uchaguzi huo.

LDP pia haikugombea katika eneo namba 3 mkoani Nagasaki. Uchaguzi huo mdogo ulifanyika kwa sababu mbunge alijiuzulu kutokana na kashfa ya uchangishaji fedha za kisiasa.

Chaguzi hizo ndogo ni za kwanza tangu kashfa ya uchangishaji fedha ya chama cha LDP kuwa hadharani msimu wa pukutizi mwaka jana. Mapema mwezi huu, LDP iliadhibu makumi ya wanachama ambao walipata mapato kutokana na mauzo ya tiketi za kuchangisha pesa lakini hawakutangaza ipasavyo mapato hayo.