Urusi yalenga mitambo ya nyuklia ya Ukraine, Ukraine yashambulia vituo vya kusafisha mafuta vya Urusi

Wizara ya nishati ya Ukraine ilisema kuwa jeshi la Urusi limeshambulia vituo vya nishati katika eneo la Dnipropetrovsk mashariki mwa Ukraine na maeneo mengine juzi Ijumaa usiku hadi jana Jumamosi asubuhi na kuharibu kwa kiasi kikubwa mitambo minne ya nishati.

Katika hatua nyingine jeshi la Ukraine limefanya shambulizi katika vituo vya kusafisha mafuta nchini Urusi.

Shirika la habari la Urusi Interfax liliripoti kuwa shughuli katika mtambo mmoja katika eneo la Krasnodar nchini humo zilisitishwa kwa sehemu kufuatia shambulizi la droni la Ukraine.

Chombo kimoja cha habari cha Ukraine kilikinukuu chanzo kimoja cha kiintelijensia kikisema kwamba usalama wa taifa wa nchi hiyo ulifanya shambulizi hilo.

Wakati Urusi ikiendelea na uvamizi wake wa kijeshi nchini Ukraine, chombo huru cha habari cha Urusi cha Verstka Alhamisi wiki hii kiliripoti kuwa makosa mengi ya kihalifu yamekuwa yakifanywa na wanajeshi ambao walirejea kutoka katika vita nchini Ukraine.

Kimesema kwamba taarifa za umma kutoka katika ripoti za habari na rekodi za hukumu zilijumlishwa na visa 55 vya mauaji ambapo watu 76 waliuawa, vilifanywa na wanajeshi wa zamani katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Kampuni moja binafsi ya kijeshi ya Wagner Group ilisemekana kuajiri wafungwa ili wapigane katika vita dhidi ya Ukraine, wakiwaambia kwamba watasamehewa ikiwa watapigana kwa kipindi cha miezi sita.

Ripoti hiyo inasema kwamba waathirika 44 wa mauaji waliuawa na wafungwa wanajeshi wa zamani waliosamehewa kifungo.

Chombo hicho cha habari kinasema kwamba idadi ya makosa kama hayo inaweza kuwa kubwa zaidi.