Wimbi la joto kali laua watoto wasiopungua wawili

Wimbi la joto kali linaloendelea, linawaathiri watu zaidi ya milioni mbili wanaoishi katika mazingira magumu kwenye Ukanda wa Gaza, na limesababisha vifo kadhaa wakiwemo watoto.

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kutoa misaada na Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina Mashariki ya Kati UNRWA Philippe Lazzarini aliandika kwenye mitandao ya kijamii juzi Ijumaa kwamba “watoto wasiopungua wawili wamekufa kutokana na joto kali.”

Aliongeza kuwa, “Ni nini zaidi cha kuvumilia: kifo, njaa, ugonjwa, kuhamishwa na sasa kuishi katika vibanda vya kukuzia mimea chini ya joto kali.”

Lazzarini, alisisitiza tena wito wake wa kusitisha mapigano kwa kuandika, “Hatuwezi kumudu zaidi ya hali hii ngumu, operesheni kubwa ya kijeshi inaendelea.”

Mamlaka za afya kwenye eneo hilo la ukanda lililozingirwa zinasema zaidi ya watu 34,000 wameuawa katika kipindi cha miezi sita tangu mzozo huo mbaya ulipoanza.

Vyombo kadhaa vya habari vimeripoti kwamba joto lilikuwa takribani nyuzijoto 30 za Selisiyasi katika siku za hivi karibuni, juu zaidi ya kiwango cha kawaida kwa wakati huu wa mwaka.