Hafla zafanyika kuadhimisha miaka 38 ya ajali ya kituo cha nyuklia cha Chornobyl

Hafla ilifanyika huko kaskazini mwa Ukraine juzi Ijumaa kukumbuka watu waliofariki kwenye ajali ya nyuklia ya Chornobyl.

Baada ya washiriki kuweka maua kwenye mnara wa makumbusho, Oleh Bondarenko, mwenyekiti wa kamati ya sera ya mazingira ya baraza la kamati kuu ya Ukraine, aliwapongeza wale waliozima moto kwenye mtambo wa Chornobyl, akisema hatua hiyo iliiokoa dunia kutoka kwenye janga la mionzi.

Rais Volodymyr Zelenksyy wa Ukraine aliandika kwenye mitandao ya kijamii siku hiyo hiyo kwamba “Ni jukumu la dunia nzima kuishinikiza Urusi” kuhakikisha kwamba kituo cha nyuklia cha Zaporizhzhia kinakuwa huru, na kwamba vituo vyote vya nyuklia vya Ukraine vinalindwa. Alisema, “Hii ni nja pekee kuzuia majanga mapya ya mionzi.”

Mapema mwezi Aprili, mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia ulishambuliwa kwa siku tatu mfululizo.

Urusi inasema mashambulio yalifanywa na vikosi vya Ukraine kwa kutumia droni. Lakini Ukraine inasema Urusi ilifanya operesheni hiyo kwa kuficha utambulisho wake ili kufanya ionekane kwamba Ukraine inahusika.