Korea Kaskazini yasema itaendelea na jukumu lake la kufuatilia anga za juu

Korea Kaskazini inasema itaendelea na “jukumu lake muhimu,” kama lilivyopangwa, kufuatilia shughuli za kijeshi za Marekani na vikosi vingine vya adui ili kuimarisha uwezo wake wa uchunguzi angani.

Nchi husika zipo katika hadhari ya juu kwani Korea Kaskazini inaaminika kujiandaa kwa urushaji wa satelaiti nyingine ya uchunguzi wa kijeshi katika siku za hivi karibuni.

Korea Kaskazini ilibainisha mipango ya kurusha satelaiti zingine tatu za uchunguzi wa kijeshi mwaka huu, kufuatia kile ilichokiita urushaji uliofanikiwa wa satelaiti yake ya kwanza ya kijeshi, Malligyong-1, mwezi Novemba mwaka jana.

Msemaji wa Mamlaka ya Taifa ya Teknolojia ya Anga za Juu ya Korea Kaskazini, yenye jukumu la kurusha satelaiti za uchunguzi wa kijeshi, ilitoa taarifa yake kupitia shirika la habari linaloendeshwa na serikali la Korean Central News Agency jana Jumamosi.

Mamlaka hiyo ilikosoa urushaji wa pili wa satelaiti ya uchunguzi ya Korea Kusini kutoka Marekani mwezi huu, na kusema mradi wa maendeleo wa Korea Kaskazini, ikiwemo urushaji wa satelaiti ya kijeshi, ni "chaguo muhimu la kimkakati kuhakikisha usalama wa nchi hiyo, maslahi na haki ya kuwepo."

Shirika la ushauri wa kitaalam la Marekani linasema picha za satelaiti za kituo cha Korea Kaskazini cha kurushia satelaiti cha Sohae kilichopo kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, zinaonyesha kwamba maandalizi yanaendelea yakifuatiwa na urushaji mwingine wa satelaiti ya uchunguzi katika siku za usoni.