Viongozi wa vyama vya wafanyabiashara Japani waelezea wasiwasi juu ya yeni dhaifu kufuatia uamuazi wa Benki Kuu ya Japani

Viongozi wa biashara nchini Japani wameongeza kutoa wito kwa viongozi wa Benki Kuu ya Japani BOJ, kufanya marekebisho baada ya thamani ya yeni kushuka zaidi dhidi ya dola jana Ijumaa. Kushuka huko kumefuatia uamuzi wa BOJ kuendeleza sera yake ya fedha bila kubadilika.

BOJ iliamua kudumisha sera iliyoianzisha mwezi Machi mwaka huu, pale ilipoondoa viwango vya muda mfupi kutoka kiwango cha asilimia sifuri hadi 0.1. Benki hiyo inasema itadumisha lengo hilo.

Gavana wa BOJ Ueda Kazuo alisema kwenye mkutano na wanahabari jana Ijumaa kwamba yeni dhaifu haijaleta athari kubwa kwenye kiwango cha mfumuko wa bei wa Japani.

Alisisitiza tena maoni yake kwamba BOJ inatarajiwa kuendeleza sera yake rahisi ya fedha kwa wakati huu.

Ueda pia alisema kwamba iwapo athari za yeni dhaifu juu ya bei ya jumla itafikia kiwango ambacho hakiwezi kupuuzwa, itachukuliwa au ikiwezekana kutumika kama msingi wa kufanya maamuzi kwa upande wa sera za fedha.

Lakini maoni yake hayakuchukuliwa kama ujumbe thabiti katika kudhibiti kushuka kwa thamani ya yeni, na kuhamasisha wawekezaji kuuza sarafu hiyo.

Huku yeni ikiendelea kushuka thamani kwa miaka 34, wafanyabiashara wanaangazia kwa kina juu ya uwezekano wa serikali na BOJ kuingilia soko.