Japani, Brazil zaangazia mpangokazi wa pande mbili wa kupunguza hewa ya kaboni

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio na Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva wamepanga kuanzisha mpangokazi mpya wa pande mbili katika nyanja ya kupunguza hewa ya kaboni.

Kishida anatarajiwa kuzuru nchini Brazil Mei 2 mwaka huu.

Lula atakuwa mwenyekiti wa mkutano wa mwaka huu wa Kundi la nchi 20 zilizoendelea zaidi Kiuchumi Duniani.

Mpangokazi huo mpya wa pande mbili utalenga katika kutumia kwa ufanisi utajiri wa rasilimali za Brazil kama vile nishati asilia na utaalamu wa Japani katika teknolojia kama ile ya injini za mseto.

Mpango huo unatarajiwa kuzishuhudia sekta za umma na binafsi za nchi hizo mbili zikiongeza kufanya kazi pamoja.

Brazil inatarajiwa kuwa mwenyeji wa kongamano la mwaka la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi mwaka ujao.

Aidha Brazil inatarajiwa kuchukua jukumu muhimu kwenye msukumo wa kimataifa kupunguza hewa ya kaboni.