Maswali na Majibu: Magonjwa ya kupe (4)

(4) Hatua za uzuiaji: Mavazi

NHK inajibu maswali yanayohusiana na kuhakikisha usalama katika maisha yetu ya kila siku. Magonjwa yanayoenezwa na kupe wanaoishi katika maeneo ya misitu na mashamba yamekuwa yakiongezeka katika miaka ya hivi karibuni. Magonjwa haya yanaweza yakasababisha dalili kama vile homa ama kuharisha na huenda yakasababisha kifo katika baadhi ya visa. Mfululizo huu unajadili masuala ya kuzingatia na njia ya kuzuia kuumwa na kupe. Katika kipengele hiki cha nne, tunakupa vidokezo juu ya mavazi ili kuepuka kuumwa na kupe.

Unapoenda katika makazi ya kupe, kama vile mashamba yenye nyasi na vichaka, unapaswa kuvaa mavazi yenye mikono mirefu na suruali ili kupunguza kuonekana kwa ngozi kwenye mikono, miguu na shingoni. Vaa kofia na taulo shingoni. Ingiza sijafu la shati lako kwenye glavu, pindo la shati lako kwenye suruali na pindo la suruali yako kwenye buti au soksi ili kufunika nafasi yoyote kati yake. Haushauriwi kuvaa kaptura na ndara. Unapokuja nyumbani, vua mavazi ya nje kabla ya kuingia kwenye nyumba na angalia ikiwa kuna kupe. Tumia utepe unaonata kuondoa kupe yeyote ambaye atapatikana. Pia wakati wa kuoga, angalia makwapani na sehemu zingine za mwili kubaini ikiwa umeumwa na kupe.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Aprili 26, 2024.