Blinken awasilisha wasiwasi wake kwa China kama inavyodaiwa kusaidia sekta ya ulinzi ya Urusi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken anasema ameelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya China inavyodaiwa kusaidia sekta ya ulinzi ya Urusi wakati wa majadiliano yake na viongozi wa China.

Blinken alitoa maoni hayo kwenye mkutano wake na wanahabari jijini Beijing nchini China jana Ijumaa baada ya kufanya mikutano na Rais wa China Xi Jinping na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi.

Blinken alisema wakati Marekani ikiangazia kuimarisha ushirikiano na China pale maslahi ya nchi hizo yanafungamana, Marekani “inatambua hatari zinazowekwa” na China na "maono yake ya kushindana kwa siku zijazo."

Alishauri kwamba Marekani inaweza kuiwekea China vikwazo zaidi kutegemea na jinsi nchi hiyo itakavyochukua hatua juu ya inavyodaiwa kusaidia sekta ya ulinzi ya Urusi wakati huu wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Blinken alisema nchi hizo mbili pia zilijadili shughuli za baharini za China kwenye Bahari ya China Kusini.

Alisema kuwa wakati Marekani ikiendelea kufanya kazi kupunguza mivutano, "ahadi yake ya ulinzi kwa Ufilipino itasalia bila kubadilika."

Alisema kwamba pia alisisitiza juu ya umuhimu wa amani na uthabiti kwenye Mlango Bahari wa Taiwan.